Hatimaye mwanajeshi aliyeuliwa na wanamgambo wa Alshabaab kule El Adde Somalia wakati wa shambulizi kwenye kambi ya wanajeshi wa Kenya, Simon Maoga amezikwa nyumbani kwao katika kijiji cha Bobembe, eneo bunge la Mugirango.
Akihutubu kwenye hafla hiyo siku ya Jumanne, wakili wa masuala ya sheria Steve Mogaka aliitaka serikali kufidia familia ya mwendazake kwa kuajiri mtu mmoja kutoka familia hiyo ili kuhudumu jeshini.
"Leo tunamzika jamaa aliyejitolea kulinda taifa letu kutokana na mashambulizi ya magaidi na kwa maana hii ni safari ya mwisho wa shujaa huyu tunaiomba serikali ya kitaifa ifanye mpango wa kuajiri mtu mmoja wa familia hii kwenye jeshi kama njia mojawapo ya kuwafidia waliofiwa," alisema Mogaka.
Mogaka aidha alisema kuwa yafaa serikali iwaondoe wanajeshi wake nchini Somalia na kisha kuimarisha usalama kwenye mipaka ili kuzuia mashambulizi zaidi nchini.
"Taifa hili limekuwa likipigana na wanamgambo wa Alshabaab kule Somalia kwa miaka minne sasa lakini wangali wanatushambulia na ndio maana naona ingekuwa bora iwapo serikali ingewaondoa wanajeshi wake nchini Somalia na kuimarisha usalama mipakani," aliongezea Mogaka.