Wakili wa Feisal Mohamed, anayekabiliwa na shtaka la ulanguzi wa pembe za ndovu ameitaka mahakama kutupilia mbali kesi hiyo.
Wakili Gikandi Ngubuini, aliwasilisha ombi hilo la kutaka kesi hiyo itupiliwe mbali siku ya Ijumaa, kwa madai kuwa afisi ya mkurugenzi mkuu wa mashtaka ya umma inajikokota katika kuendesha kesi hiyo, bila sababu za kutosha.
Gikandi alidai kuwa naibu mkurugenzi mkuu wa mashtaka ya umma tawi la Mombasa, Alexendra Muteti, ameshindwa kuwasilisha mashahidi zaidi ili kuharakisha kusikizwa kwa kesi hiyo, ili haki na usawa kupatikana kwa mteja wake.
Hata hivyo, Muteti alipinga madai hayo na kusema kuwa afisi yake iko tayari kuendelea na kesi hiyo wakati wowote.
Kufikia sasa, mashahidi watisa ndio wametoa ushahidi akiwemo aliyekuwa mkuu wa polisi wa Makupa Peter Mbua.
Mohamed na wenziwe wanakabiliwa na shtaka la ulanguzi wa pembe za ndovu 314.
Mahakama itatoa mwelekeo kuhusu kesi hiyo Novemba 23, 2015.