Wakili Kemosi Mogaka amewataka vijana katika kaunti ya Nyamira kujitokeza kujisajili ili kupokea vitambulisho.
Akihutubia wanahabari mjini Nyamira siku ya Ijumaa wakati wa kuwapokeza wanafunzi 50 waliofanya vyema kwenye mtihani wa darasa la nane hundi ya shillingi elfu 300,000, Mogaka alisema kuwa ili vijana kufanya maamuzi kwenye chaguzi mbalimbali sharti wachukue vitambulisho.
“Sharti vijana wajitokeze kujisajili kupata vitambulisho vya kitaifa ili wajisajili kupata kadi za kupiga kura kwa kuwa kura ndio zitawawezesha kufanya maamuzi ya busara kwenye uchaguzi mkuu ujao, na kwa kweli hiyo ndio njia ya kipekee ya kuwachagua viongozi bora,” alisema Mogaka.
Mogaka aidha aliwahimiza vijana kuasi tabia ya kununuliwa na wanasiasa ili kuwapigia kura akihoji kuwa hali hiyo itaendelea kurudisha nyuma taifa kimaendeleo.
“Iwapo tutaendelea kukubali kununuliwa na wanasiasa ili kuwapigia kura, wacha tujue kuwa kamwe hili halitaimarika kiuchumi maana tutawachagua viongozi wasio stahili kuwa mamlakani na kwa maana hiyo tutasalia nyuma kimaendeleo,” aliongezea Mogaka.