Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Ukabila unafanya watu wachaguane kama vipofu, na kusalia maskini kwa miaka mitano, amesema wakili Karanja Kabage.

Akizungumza katika kanisa la Full Gospel Revival Centre Bahati mnamo Jumapili, Kabage aliwataka wakaazi wa kaunti ya Nakuru kuchagua watu wa kuwasaidia, ila si watu watakaonyakua nyadhifa ili wajisaidie wenyewe.

“Tatizo letu kama wakenya ni kwamba, tunachagua mtu hata ambaye hana rekodi ya maendeleo, mradi tu amekupa shilingi mia ama hamsini, unamchagua. Ufisadi huu wakati wa uchaguzi, hukufanya wewe kuwa mtumwa, maskini na mtu hohe hahe kwa miaka mitano,” Karanja Kabage alisema.

Kabage tayari ametangaza nia ya kuwania useneta katika kaunti hio.

Aidha alisema Nakuru inahitaji mtu wa kuitetea katika serikali kuu kifedha, na wakati nafasi za kazi zinapotokea, akijitangaza kama mwenye uwezo huo.

Alisema kwamba: “Watu wa Nakuru wanataka seneta mkakamavu, seneta jasiri, atakayekosoa ubadhirifu wa pesa kutoka kwa wabunge, atakayekosoa na kulainisha matumizi mabaya ya pesa katika serikali ya kaunti, na japo huu si wakati wa siasa, mimi nasema wakati huo ukifika mnipe nafasi hiyo, nina uwezo.”