Share news tips with us here at Hivisasa

Shughuli za usafiri kwenye barabara kuu ya Nairobi kuelekea Nakuru zilitatizika Jumatano adhuhuri baada ya maelfu ya wakimbizi wa ndani kwa ndani kuandamana wakielekea mjini Nairobi.

Takriban wakimbizi 2,500 kutoka eneo la Olkalou walifunga safari kuelekea ikulu ya Nairobi ambapo walipania kukutana na Rais Uhuru Kenyatta ili kumwelezea masaibu yao.

Msafara huo ulisababisha msongamano mkubwa wa magari hususan eneo la Gilgil huku baadhi ya wakimbizi hao wakiweka mawe na miti barabarani kufunga barabara hiyo.

Hata hivyo, azma ya waadhiriwa hao wa machafuko ya baada ya uchaguzi wa mwaka 2007 ya kufika Nairobi ziliambulia patupu baada ya polisi wa kuzima ghasia kuwatupia vitoa machozi huku baadhi yao wakipata majeraha.

“Tumekuwa kambini sasa kwa miaka minane, na hatujapewa fidia wengine wakipatiwa. Tunataka mashamba yetu tuliyonyaganywa yarudishwe kama fidia,” alisema mmoja wao, Solomon Macharia..

Walioumia na kupelekwa hospitali kuu ya wilaya ya Gilgil kufuatia purukushani hizo, ni ikiwemo wazee na watoto.

Hii sio mara ya kwanza kwa wakimbizi hao kujaribu kuandamana hadi ikulu, kwani mwaka wa 2014 walifanya maandamano mengine eneo hilo lakini yakakatizwa na polisi.