Zaidi ya wakimbizi 100 wa ndani kwa ndani waliokuwa wakiishi katika eneo la Maji Matamu, Rongai kwenye kaunti ya Nakuru kabla ya machafuko yaliyojiri baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka wa 2007 sasa wanaitaka serikali kuwajumwishwa kwenye orodha ya wale wanaofaa kufaidi kutokana na sehemu ya pili ya mpango wa kuwapa fidia wakimbizi wa ndani kwa ndani.
Wakizungumza na wanahabari huyu siku ya Ijumaa, wakimbizi hao walisema licha ya kuwa na stakabadhi zote zinazohitajika katika kudihinisha ombi lao hilo, hawajapokea msaada ufaao ili kuafikia hilo kutoka kwa serikali kupitia kwa wizara husika.
Mwakilisi wa wakimbizi hao Michael Ndiba alisema wanachama wote wamepokea ilani kutoka kwa kwa kituo cha polisi cha Solai ambapo walikuwa wamekita kambi huku wakipewa pia ripoti kuhusiana na kuharibika kwa miea yao kutoka kwa shirika la msalaba mwekundu nchini wakiwa kwenye kambi hiyo.
Alisema kuwa wamewaandikia barua viongozi mbalimbali wa serikali kuhusiana na ombi lao hilo, lakini ombi hilo halijapata kuangaziwa na yeyote kufikia sasa.
Kwa sasa wameelezea hofu yao kuwa huenda wakatengwa wakati ambao shughuli ya kuwapa fidia wakimbizi wa ndani kwa ndani itakaporejelewa tena mwezi Februari mwaka ujao wa 2016.