Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Baadhi ya wakulima Muhoroni kaunti ya Kisumu, wamelalamikia kile wanachosema ni kunyanyaswa na kampuni za sukari nchini.

Wakulima hao wamesema kampuni hizo zimekuwa zikichukua muda zaidi kuwalipa pesa, baada ya kuwasilisha miwa yao.

''Kwa sasa imepita miezi 5 bila kulipwa miwa yetu, ikiwa ni kuanzia mwezi Novemba hadi Januari na kwa sasa tumefika mwezi February na hatujapokea malipo ya miwa yetu, '' alisema mmoja wa wakulima hao ambaye hakutaka jina lake kutambuliwa.

Wameongeza kuwa watoto wao wamekwama nyumbani kwa sababu ya ukosefu wa karo, kutokana na kucheleweshwa kwa malipo yao.

''Nilipeleka miwa yangu katika kiwanda cha sukari cha Chemilil mwezi Septemba na kufikia sasa sijapata pesa, wengine waliopeleka miwa yao mwezi wa Oktoba na November wamelipwa, kwa sasa watoto wangu wamefukuzwa wako nyumbani kutokana na ukosefu wa karo nilikuwa natarajia malipo kutokana na miwa ndiposa nipate kulipa karo,'' alidakia mkulima mwingine.

Wameihimiza serikali kuingilia kati swala hilo, ili kuhakikisha kuwa wanapokea malipo ya miwa yao kwa wakati.