Kikundi kimoja cha wakulima kutoka eneo la Kinangop na Naivasha wametishia kutolipa ada kwenye serikali husika kutokana na ubovu wa barabara za maeneo hayo.
Huku wakifanya maandamano ya pamoja, wakulima hao wamelalamikia hali mbaya ya barabara ya Maraigushu-Githabai-Githioro ambayo kwa sasa haipitiki.
Haya yamejiri huku ripoti zikiibuka kuwa chakula cha mashamba yao cha dhamani kubwa kilikuwa kikiharibika kwani magari hayaingii kukichukua ili kukipeleka sokoni.
Mmoja wao Gilbert Mwangi amesema kuwa wabunge wa Naivasha na Kinangop John Kihagi na Stephen Kinyanjui mtawalia walikuwa wamekosa kuwajibika katika kazi zao.
“Tumepeleka malalanishi yetu kuhusu barabara hii lakini viongozi wetu hakuna hatua wamechukua hadi kufikia sasa, ikiwa hatutasikizwa basi tutakaidi kulipa ushuru,” alisema Bw Kinyanjui.
Mwangi amesema kuwa walikuwa wamelalamikia serikali za kaunti ya Nyandarua na Nakuru lakini vile vile hakuna hatua iliyochukuliwa.
Naye Bi Agatha Murugi ameonya kuwa hawatalipa ada kwa serikali hizo hadi pale barabara hizo zitatengenezwa ili waweze kuendelea na shughuli zao kama kawaida.
“Hatutalipa ada kwa serikali ya kaunti ikiwa barabara hii haitatengenezwa, tumeenda hasara kubwa sana kwa sababu ya kutotengenezwa kwa barabara hii,” alisema Bi Agatha.