Baadhi ya wakulima wanaokuza chai kutoka wadi ya Gesima wameiomba kamati ya maendeleo ya eneo bunge la Kitutu Masaba kuwapa msaada wa pesa zitakazowawezesha kumaliza kituo cha kupimia chai katika eneo hilo.
Wakiongea katika kituo cha kupimia chai cha Riaking'oina kwenye mkutano waliouandaa ili kuweka mikakati ya kutafuta njia ya kupata pesa zitakazowasaidia kukarabati kituo hicho, wakulima hao wamesema kuwa njia tu ya kufadhili mradi ni kupitia hazina ya maeneo bunge la Kitutu Masaba.
Wakiongoza na mwenyekiti wao Jackson Atera wakulima hao wamesema kuwa inafaa kamati ya ustawishaji wa maeneo bunge kwenye eneo la uwakilishi la Kitutu Masaba kutengea pesa vituo vya kupimia chai.
“Tunaiomba kamati ya ustawishaji wa maendeleo bunge la Kitutu Masaba kutusaidia pesa ili tuwe na mahali pazuri pa kupimia mazao yetu kwa kuwa tunategemea sana chai kupata mapato yetu,” alisema Atera.
Atera ameongeza kwa kusema kuwa kwa muda sasa wamekuwa wakisihi kamati hiyo kuwatengea pesa bila mafanikio, na akaongeza kwa kuwahimiza wakulima wasife moyo kukuza zao hilo kwani ndilo wanalo litegemea kuendeleza maisha yao.
“Kwa muda sasa tumekuwa tukitafuta msaada kutoka kwa kamati hiyo bila mafanikio ila nawasihi wakulima wasife moyo kukuza zao la chai kwa kuwa ndilo tunalo litegemea,” alisema Atera.