Wakulima wa mmea wa Pareto kutoka kaunti za Nyandarua, Lakipia na Nakuru wametishia kususia uchaguzi ujao wa mwaka 2017 iwapo serikali haitawalipa madeni yao ili kuokoa sekta hiyo ambayo inaelekea kudidimia.
Wakizungumza na wanahabari jijini Nakuru siku ya Ijumaa, wakulima hao kupitia mwenyekiti wao Julius Njogu wameelezea kuwa wanadai serikali takriban milioni 863 ambazo hawajilipwa kwa kadri miezi mine na mitano.
"Ni jambo la kusikitisha kuona serikali imetumia shilingi milioni 300 kila mwaka tangu mwaka 2013 ilhali wakulima bado hawajalipwa mishahara yao ya miezi minne na mitano. Tunamwomba Rais Uhuru Kenyatta kuingilia kati suala hili ili kuokoa wakulima katika sekta hii, la sivyo hatutahusika katika uchaguzi ujao," Njogu alilalama.
Bwana Njogu pia ameelezea kuwa malipo ya maua waliyouza mwaka 2013 na 2014 bado hayajalipwa huku pia akiiomba serikali kuwapa wakulima mashamba ya kupanda mmea huo.
"Tunaiomba serikali kutupa mashamba ya pareto yaliyoko Bahati, Molo, Oljororok na Mawingu ili tuyauze mazao yetu kwa sekta za kibinafsi. Hili litawezesha wakulima kuzoa faida nyingi katika ukulima wa mmea huo," Njogu alielezea zaidi.