Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Wakulima wa viazi wilayani Molo na Kuresoi wamelalamikia bei duni ya zao la viazi huku wakisema wanunuzi wamekuwa wakikiuka sheria ya upakiaji wa viazi kwa kilo 50.

Wakulima hao wameeleza jinsi wanavyokadiria hasara kubwa licha ya kuwekeza fedha nyingi katika ukuzaji wa viazi, huku wakikosa soko tayari kwa zao hilo.

Wamesema kwa miaka mingi madalali wamekuwa wakiwakandamiza na kuwasababishia hasara kubwa.

“Sheria ilipitishwa kwamba tutakuwa tukinunuliwa viazi kwa kilo, lakini sasa bei imekuwa chini sana hata kuliko ilivyokuwa mbeleni,” alisema Margaret Muthoni, mkulima wa viazi.

Kwa sasa wakulima hao wameitaka serikali kuwanunulia viazi vyao na kumiliki sekta hiyo, sawia na sekta ya maziwa chini ya kampuni kama KCC.

“Hapa kwetu Molo kuna vyakula vingi, na serikali inafaa kutununulia chakula hicho ili kuwapelekea wale ambao hawana kwa sababu hatuna soko,” alisisitiza.