Share news tips with us here at Hivisasa

Wakulima kaunti ya Nakuru wameitaka serikali kupitia kampuni ya mbegu nchini (Kenya Seed) kufanya msako na kupigana na mbegu haramu ambazo wanadai zimejaa sokoni.

Wakiongea Jumatatu ,wakulima kutoka eneo bunge la Molo wamesema kuwa mbegu bandia zilizo na nembo ya shirika la kukadiria ubora wa bidhaa nchini (KEBS) zimetapakaa madukani.

Wakiongozwa na mwenyekiti wa chama cha wakulima na ushirika cha molo Bernard Mwega,wakulima hao wamesema kuwa uwepo wa mbegu hizo ni hatari kwa wakulima kwani huenda zitawaletea hasara kubwa.

“Kuna mbegu nyingi sana sokoni ambazo si halali,na zina nembo ya KEBS na Kenya seed na tunaitaka serikali na Kenya seed pamoja na KEBS wafanye msako katika maduka yote ya mbegu ili wanase mbegu hizo haramu,” alisema Mwega.

“Wakulima wengi hawawezi tofautisha kati ya mebgu halali an haramu na ni jukumu la serikali kuwaepushia hasara kwa kuhakikisha kuwa mbegu hizi zimeondolewa sokoni,” aliongeza.

Rachael Wamae ambaye ni mkulima katika eneo la Molo alielezea hasara wakulima wengi walioipata msimu uliopota kwa kupanda mbegu haramu.

“Wakulima wengi sana walipata hasara kubwa sana msimu jana kwa kuwa tulinunua mbegu kumbe zilikuwa haramu na hakuna mavuno tuliopata na hatutaki hilo litokee tena,” alisema.

Wakulima hao waliitaka kampuni ya Kenya seed kuhakikisha kuwa ni wauzaji waliosajiliwa na kuidhinishwa pekee wanaoruhusiwa kuuza mbegu kwa wakulima illi kuepusha tabia ya wakulima kuuziwa mbegu bandia.