Share news tips with us here at Hivisasa

Idadi kubwa ya wakulima eneo la Nyanza wameomba serikali kuwasambazia mbolea na mbegu ya kupanda mapema kabla ya muda wa upanzi kuyoyoma na kusababisha mazao duni.

Hii ni baada ya wengi wa wakulima kumaliza matayarisho ya mashamba yao katika Kaunti ya Kisii na ile ya Nyamira huku wakiomba Wizara ya Kilimo kufanya mipango ya mapema ili kuwapa bidhaa hizo.

Wakulima hao walisema hawataki mapato au mavuno duni ikilinganishwa na msimu uliopita kutokana na kuchelewa kufanya upanzi wao.

Wakiongea na mwandishi huyu siku ya Ijumaa katika eneo la Itare, wakulima hao waliomba serikali kuwajali na kuwakabidhi mbolea mapema.

“Tunaomba serikali kutusambazia mbolea na mbegu mapema ili tufanye upanzi maana tunapochelewa, mavuno huwa duni zaidi na kusababisha janga la njaa katika maeneo yetu ya Kisii,” alihoji Irene Kerubo.

Kerubo pia alisema kuwa amemaliza kuandaa shamba lake pamoja na mbegu na yupo tayari kwa upanzi wakati anaposubiri kuletewa mbolea na mbegu hizo.

Katika sehemu zingine za kaunti hizo shughuli za kuandaa mashamba zinaendelea huku ili kufanya upanzi wao na kutarajia mavuno bora.

“Wengine tunaendelea kutayarisha mashamba na tuko karibu kumaliza, tunaomba serikali isichelewe kama wakati uliopita kwa kutusambazia mbegu na mbolea,” alisema Nickson Mochama, mkulima mwingine.