Wakulima katika maeneo bunge ya Subukia na bahati wametakiwa kurejelea kilimo cha pareto kama njia moja ya kuinua viwango vya maisha yao.
Mtaalamu wa kilimo cha pareto kaunti ya Nakuru George Kigoro amewataka wakulima wote waliokiasi kilimo cha pareto kufikiria upya kuhusu uamuzi wao na kuanza tena kupanda zao hilo.
Akiongea wakati wa shuguli ya uhamasisho kuhusu kilimo cha pareto katika eneo bunge la Subukia hapo jana,Kigoro alisema kuwa kilimo cha pareto kimefufuliwa na kuwa kina faida kubwa kushinda hapo awali.
“Watu wengi hapa walikuwa wakipanda pareto lakini waliacha baada ya sekta hiyo kuporomoka lakini sasa serikali ya kitaifa na ya kaunti imerejesha sekta ya pareto inapostahili kuwa na ndiposa tuko hapa kuwarai nyinyi kurejelea upanzi wa pareto,” alisema Kigoro.
Kigoro aliongeza kuwa kama njia moja ya kufufua sekta ya pareto serikali itatoa mafunzo, mbegu, mbolea na soko la bidhaa hiyo kwa kila mkulima atakaye kumbatia kilimo hicho.
“Kama kuna anataka kupanda pareto basi serikali iko tayari kukupa mbegu za bure, mbolea na mafunzo na baada ya kuvuna tutahakikisha kuwa unapata soko tayari kwa zao lako,” akasema.
Afisa wa kilimo katika kaunti ndogo ya subukia Nicholas Nderitu aliwata wakulima wanaotaka kurejelea upanzi wa pareto kujiandikisha na afisi yake ili waweze kufadhiliwa na serikali.
“Wale wote ambao wako tayari kupanda pareto waje katika afisi yetu na tutawapa usaidizi wote wanaohitaji,” alisema.