Baada ya rais Uhuru Kenyatta kutangaza kuwa serikali itatoa shilingi milioni 400 kufufua kiwanda cha KCC wakulima North-Rift wanataka pesa hizo kutolewa kabla ya mwisho wa mwaka huu.
Watetezi wa maswala ya wakulima kutoka eneo hilo walisema mara kwa mara serikali imekuwa ikitoa ahadi ya kufufua kiwanda hicho ambapo utekelezaji wa ahadi husika huwa haufanyiki kwa wakati.
Wakiongozwa na Kipkorir Menjo walisema iwapo ahadi hiyo itatekelezwa kwa wakati itakuwa afueni kwa wakulima wafugaji wa ng’ombe wa maziwa. Menjo alisema sekta ya uzalishaji maziwa inahitaji kupigwa jeki ili kuifufua ikizingatiwa kuwa inatishiwa kuangamia.
“Tunashukuru rais kwa msaada huo lakini tunatoka kuona kwa vitendo kabla ya mwisho wa mwaka huu ili wakulima lengwa wanufaike” alisema Menjo.
Kiongozi huyo alionya dhidi ya hatua zozote za kubinafsisha kiwanda hicho.
Menjo alidai kuwa kuna mabwenyenye fulani ambao wananjama ya kubinfsisha kiwanda hicho kwa manufaa yakibinafsi. Wakulima kwa pamoja walisema watatumia kila mbinu kupinga njama kama hiyo.
Kuhusu hatua ya rais Kenyatta kuahidi kutolewa kwa shilingi milioni 600 kufufua kiwanda hicho wakulima walitaka nafasi ya uajiri katika kiwanda hicho kutoa nafasi ya kwanza kwa vijana kutoka katika kaunti ya Uasin-Gishu.
Rais Kenyatta alitoa ahadi hizo hivi maajuzi alipozuru eneo la North Rift kukagua miradi ya maendeleo.