Share news tips with us here at Hivisasa

Wakulima wa majani chai katika eneo bunge la Kitutu Chache Kaskazini kaunti ya Kisii wametishia kuandamana kulazimisha kurudishiwa pesa ambazo wamekuwa wakikatwa na halmashauri ya KTDA ili kutumika kujenga kiwanda cha majani chai katika eneo la Sombogo.

Kulingana na wakulima hao wamekuwa wakikatwa pesa kwa zaidi ya miaka minne sasa huku wakiahidiwa kujengewa kiwaanda hicho jambo ambalo wamesema halionekani kuanzishwa kushughulikiwa na kusema sasa wataandamana ili warudishiwe pesa zao ambazo wamekuwa wakikatwa.

Wakizungumza na waandishi wa habari mnano siku ya Jumatano katika eneo la Sooko wilayani Marani wakulima hao wakiongozwa na mwenyekiti wa kituo cha kupima majani chai cha Sooko Wilfred Monari walisema wamekuwa wakisubiri ujenzi wa kiwanda hicho kuanzishwa rasmi katika eneo la Sombogo jambo ambalo hawalioni na kutishia kuandamana kulazimisha halmashauri ya KTDA kuwarudishia pesa zao ili kufanyia vitu za muhimu.

“Wakulima wote tulikubaliana tujengewe kiwanda chetu katika eneo la Sombogo kaunti ya Kisii kwani majani chai katika kaunti hii ya Kisii ni mengi ambayo huharibikia kwa vituo vya ununuzi kwa kutochukuliwa kwa wakati unaofaa,” alisema Monari

“Tayari shamba lilinunuliwa kwa zaidi ya miaka mitatu iliyopita katika eneo la Sombo hekari 6, hakuna ujenzi umeanzishwa hadi sasa tumekuwa tukisubiri kwa muda mrefu bila jibu,” aliongeza Monari.

“Tutaandamana ili kulazimisha halmashauri ya KTDA kuturudishia pesa zile ambazo tumekuwa tukikatwa ili kutumika kujenga kiwanda hicho ikiwa hawataanza ujenzi,” alisisitiza Monari.

Serikali ya kaunti ya Kisii hapo awali iliahidi kutoa millioni 30 kufadhili ujenzi wa kiwanda hicho hapo mbeleni.

Wakulima hao walisema wamekuwa wakikatwa shilling 3 kwa kila kilo.