Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Ujenzi wa laini ya stima ya Olkaria- Lessos- Kisumu huenda ukasimama kutokana na hatua ya shirika la Ketraco kukosa kuwafidia wakulima walioadhirika.

Kikundi hicho cha wakulima aidha kimetishia kuelekea mahakamani ili kusimamisha ujenzi huo huku kikisema kuwa hakikufidiwa kama jinsi walivyokubaliana na shirika hilo la kiserikali.

Familia hizo zinazoishi eneo la Kayole mjini Naivasha sasa zinataka makubaliano yaliyowekwa awali kuangaliwa tena huku wakisema kuwa bei ya ardhi imeongezeka maradufu.

Akizungumza na wanahabari mapema Jumatano Mwenyekiti wao Gikonyo Mariku alisema kuwa shida zao zilianza mnamo mwaka wa 2013 ambapo waliarifiwa kuwa laini hiyo ingepitia kwenye mashamba yao na watafidiwa vilivyo.

“Tuliahidiwa kulipwa asilimia 70 ya makubaliano hayo na masalio yalipwe baada ya miezi mitatu tukio ambalo halijfanyika hadi kufikia sasa,” Mariku aliongeza.

Naye Joyce Waithera amesema kuwa kucheleweshwa kwa kulipwa kwa fidia hiyo kulikuwa kumewafanya kukadiria hasara kubwa huku wakikosa kulima kwenye mashamba hayo.

“Malipo hayo yalicheleweshwa na kwa sasa tunakadiria hasara kubwa maanake hatukulima wala kupanda chochote,” alisema Bi Waithera.