Huenda mgogoro unaokumba sekta ya elimu nchini kuhusu karo ukapata suluhu ya kudumu hivi karibuni baada ya wakuu wa shule za umma nchini kukubali kwa kauli moja kuwa wataheshimu mwongozo uliotolewa na serikali.
Siku ya Jumanne wakuu hao waliaapa kutoza karo kuambatana na mwongozo uliotelewa na serikali Februari 2015 huku wakiahidi kuwapunguzia wazazi mzigo kwa kutolipisha karo kupita kiasi.
Haya yaliafikiwa katika mkutano ulioandaliwa mjini Nairobi siku ya Jumanne, na kuleta pamoja wadau wa elimu nchini akiwemo waziri wa elimu Dkt Fred Matiangi, katibu wa chama cha walimu nchini Knut Willson Sossion pamoja na muungano wa wakuu wa shule za upili KESSHA.
Mkutano huo uliitishwa baada ya wazazi kulalamikia hatua ya baadhi ya walimu wakuu kuongeza karo maradufu wakati huu ambapo wanafunzi wanarejea shuleni kwa muhula wa kwanza.
Akizungumza na wanahabari muda mchache baada ya mkutano huo, katibu wa Knut Wilson Sossion alisema kupanda kwa bidhaa muhimu kama chakula ni miongoni mwa mambo yaliyochangia kuongezwa kwa karo.
Hata hivyo, Sossion aliwataka wazazi kutokuwa na wasiwasi akidai kuwa suala hilo sasa limepata suluhu.
"Tumekubaliana kuwa hakuna shule itakayoongeza karo bila idhini ya serikali, hivyo wazazi wasiwe na hofu,’’ alisema Sossion.
Sossion pia aliitaka wizara ya elimu na tume ya huduma kwa walimu TSC kutoa pesa za kufadhili elimu ya bila malipo mapema ili kuwarahisishia kazi wakuu wa shule.