Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Huku ulimwengu ukiadhimisha siku ya wanaoishi na ulemavu, serikali ya kaunti ya Mombasa imetenga shilingi milioni 500 katika bajeti yake kwa ajili ya jamii hiyo.

Kwa mujibu wa mkurugenzi katika idara ya vijana jinsia na michezo kaunti ya Mombasa Esther Ingolo, fedha hizo zitatumika kuboresha maisha ya walemavu kupitia miradi mbali mbali.

Japo haikutajwa ni kwa njia gani fedha hizo zitatolewa, Ingolo alisema mgao huo ni kuhakikisha walemavu wanafaidika na rasilimali za kaunti kama inavyoagiza katiba.

Maadhimisho hayo mjini Mombasa yalifanyika siku ya Alhamisi katika uwanja wa Caltex, Likoni, ambapo kundi la vijana wanaotoa huduma ya kwanza kwa jamii maarufu kama Likoni Response Team wakiongozwa na Rajab Shauri waliiomba serikali ya kaunti ya Mombasa kuwasaidia ili wazidi kutoa huduma za dharura kwa wepesi zaidi kwa wananchi.

Aidha, waliongeza kuwa wanapata changamoto nyingi kama vile usafiri wanapotoa huduma ikizingatiwa kuwa hawana uwezo wa kumikili gari na baadhi ya madawa.

Vilevile walisisitiza kuwa vifaa vyao ni duni ikilinganishwa na viwango vya matukio ya ajali yanayoshudiiwa jijini.