Jamii ya watu wanaoishi na ulemavu katika eneo la Pwani imehimzwa kujitokeza kusajiliwa ili Shirika la walemavu nchini kufahamu idadi kamili ya jamii hiyo.
Kulingana na Mshirikishi mkuu wa jamii ya walemavu eneo la Pwani Hamisa Zaja, wengi wa watu wanaoishi na ulemavu katika maeneo ya mashinani wamesalia kimya na kutojihusisha katika mashirika ya walemavu, hali inayofanya iwe vigumu wao kutambulika.
Akizungumza mjini Mombasa ofisini mwake na mwanahabari huyu siku ya Jumatatu, Zaja alisema kuwa tayari zaidi ya walemavu 500 katika eneo la Malindi na 3,000 katika eneo la Kilifi wamesajiliwa.
Hata hivyo, alisema kuwa anasubiri idadi kamili kutoka mjini Mombasa na Taita ndipo wajumuishe idadi kamili katika eneo zima la Pwani.
Zaja alisema kuwa wanatarajia kusajili zaidi ya walemavu laki tano kwani tayari serikali imewatengea shilingi milioni 200 kugharamia mahitaji yao ya kila siku, pamoja na kutekeleza miradi mbali mbali ya kimaendeleo.
“Tayari serikali imetutengea shilingi milioni 200 katika hazina yetu kutumika katika kugharamia mahitaji mbalimbali ikiwemo vifaa maalum vya walemavu pamoja na kuwatekelezea miradi ya kimaendeleo. Hilo hatuwezi tukatekeleza kabla ya kufahamu idadi kamili ya watu wanaoishi na ulemavu Pwani,” alieleza Zaja.
Zaja aliahidi kuzuru mashinani na kuwahamasisha walemavu kujitokeza na kujiandikisha ili Shirika la walemavu nchini kufahamu idadi kamili ya walemavu na kutumia fedha hizo vyema katika kushughulikia mahitaji yao.
Zoezi hilo kwa sasa linaendelea mashinani na mjini ili kukusanya idadi kamili ya jamii hiyo, na kuiwezesha Shirika la walemavu nchini kuwajibikia majukumu yake kikamilifu katika kuwashughulikia walemavu na mahitaji yao muhimu katika eneo la Pwani.