Share news tips with us here at Hivisasa

Huenda walemavu wanaotumia hali yao kujinufaisha wakajipata kwenye mikono ya kisheria baada ya idara ya kushughulika masuala ya watu wanaoishi na ulemavu kupitia katika wizara ya Vijana, Jinsia na Michezo kusema kuwa wataunda sera na sheria ambazo zitawashtaki walemavu hao.

Kulingana na mkurugenzi mkuu katika idara ya watu wanaoishi na changamoto za mwili, Esther Ingolo, baadhi ya watu walio na ulemavu wamekuwa na mazoea ya kupata msaada kutoka kwa serikali kuu kama vile pesa na magari ya magurudumu, lakini uuza na kuweka pesa mifukoni ambapo wanarudi kando ya barabara na kuombaomba hela kutoka kwa watu na waendesha magari.

Akiongea siku ya Jumanne kwenye ofisi yake na mwandishi habari huyu, Ingolo aliongeza kuwa japokuwa wana changamoto za kukabiliana na visa kama hivyo, amedokeza kuwa wanatumia sera za serikali kuu ili kuwakabili watuhumiwa mbali na kuwa bado hakujakuwa na utaratibu wa sawa wa kisheria kwa adhabu dhidi ya wanaokosa.

Mkurugenzi huyo alisema kuwa tayari kuna mipango ya kuanza kutathmini na kuweka idadi ya walemavu wote wanaoishi kwenye Kaunti hiyo, ambapo mafisa wao watapita kila wiyala zote za Kaunti ya Mombasa ili kubaini mahitaji kamili na hesabu kamili ya walemavu.

“Tutachukua data kutoka kila kaunti ndogo ili kuwa na idadi kamili ya watu walio na ulemavu, sababu bila kufanya hivyo hatuwezi kujua idadi kamili pia viwango vyao vya elimu, na kama wana kazi au la,” aliongeza Ingolo.