Share news tips with us here at Hivisasa

Walemavu katika Kaunti ya Mombasa hasa wale wenye shida ya kuongea wameitaka serikali kuu na ile ya kaunti kuajiri watafsiri wa ishara katika afisi za huduma za umma ili kuwasaidia katika kupata huduma wanazohitaji.

Akizungumza siku ya Jumane na mwanahabari wetu kwa niaba ya walemavu wote nje ya jengo la Huduma Centre jijini Mombasa, mtafsiri wa ishara Catherine Matara alisema walemavu wanapata changamoto kubwa katika kupata huduma kutoka kwa afisi za umma.

Matara aliongeza kuwa maafisa katika afisi hizo hawawezi kuwasiliana vyema na kutoa huduma kwa walemavu hao.

Wakati huo huo, wameitaka idara ya usalama kuweka usalama wa kutosha katika eneo la Posta, hasa katika kituo cha Huduma Centre kwani hapo ndipo kuna walemavu wengi wanoendeleza biashara zao.

Kauli hii inajiri baada ya walemavu hao kulalamikia kuporwa mali zao na vijana wa kurandaranda mitaani.