Waziri katika kitengo cha michezo, vijana na jinsia katika Kaunti ya Mombasa Mohamed Abbass amewata wakazi walio na ulemavu kujitokeza na kupata msaada wa serikali ili kujiendeleza kiuchumi.
Waziri huyo alisema kuwa wizara yake inalenga kufikia kila mmoja aliye na upungufu wa kimwili kama njia moja ya kuwawezesha walemavu kuwa na mbinu ya kuwa imara kiuchumi.
Akiongea mjini Mombasa siku ya Jumatatu katika hafla moja ya kuwakabidhi hela za msaada makundi mbali mbali ya watu wanaoishi na ulemavu katika Kaunti ya Mombasa, Abbas alidokeza kuwa mradi huo wa kutoa msaada wa kifedha unalenga kila kundi na watu binafsi walio na ulemavu.
Alisema kufanya hivyo ni kuwapa moyo walemavu ili wajihisi kuwa wanatambulika na serikali, na kuwafaa wale walio na azimio la kibiashara kupata nafasi hiyo ya kujiendeleza.
Waziri huyo aliwataka wakazi wa Kaunti ya Mombasa kutowabagua walemavu wenye jamii na kutoa msaada kwa watu kama hao iwapo wanahitaji na kuongeza kuwa jamii itakuwa katika nafasi mhimu, na walemavu hawatakuwa na ugumu wa kujiendeleza kama kila mmoja atachukua jukumu la kuwatambua.