Imebainika kwamba walemavu wengi hawana vitambulisho, huku walio navyo vikiwa ni vile vya kizazi cha kwanza ambavyo havitumiki katika kupiga kura.
Walemavu hao katika kaunti ya Nakuru, waliokongamana siku ya Jumatano katika uwanja wa shule ya msingi ya Kiamaina, walimtaka mbunge wa eneo bunge la Bahati Onesmus Kimani kuhakikisha kwamba walemavu wanapelekewa huduma za kuchukua vitambulisho nyumba baada ya nyingine.
“Wengine hatuwezi hata kutoka nyumbani kwa sababu ya matatizo ya kutembea. Tuletewe maafisa wa vitambulisho kila nyumba,” alisema Simon Wanjiru kutoka wadi ya Dundori, ambaye husafiri kwa kiti cha magurudumu baada ya kuumia uti wa mgongo alipoangukiwa na gogo la mti.
Naye mama Jane Wangui, ambaye hushona nguo katika kituo cha kibiashara cha Maili Nne, alilalamikia ‘madharau kwenye baadhi ya ofisi za serikali’.
“Ofisi nyingi za serikali zimo kwenye orofa katika baadhi ya majumba ya mjini, na hazina mifumo ya kuwasaidia walemavu kuyafikia,” alisema Wangui.
Afisa kutoka idara hiyo ya vitambulisho alisema kuchelewa kwa vitambulisho hutokana na hali kwamba ni mashine moja tu ambayo huchapisha vitambulisho jijini Nairobi.
“Kama kaunti ama kila eneo bunge linaweza kununua mashine moja tu, tutaweza kuwafikia hata kwa nyumba yako,” alisema afisa huyo.
Afisa huyo aidha aliongeza kuwa wanashirikiana na maafisa wa tume ya uchaguzi na mipaka nchini IEBC ili kuhakikisha kwamba wakenya wengi wanachukua vitambulisho na wakati uo huo kujiandikisha kama wapiga kura.
“Wale ambao mna vitambulisho vya zamani ama vya kizazi cha kwanza, mje mbadilishe vitambulisho hivyo tuwape vya kizazi cha sasa,” alisema afisa huyo.
Kulingana na takwimu katika eneo bunge la Bahati lina walemavu wasiopungua mia tisa, ikiwa ni la pili kutoka lile la Njoro lenye walemavu zaidi ya 1,100.