Share news tips with us here at Hivisasa

Viongozi wa chama cha KNUT, tawi la Masaba, Kaunti ya Nyamira, wamesema kuwa wana imani kuwa mahakama kuu nchini, itabadili maamuzi ya mahakama ya rufaa, kuhusu nyongeza yao ya mishahara ya kati ya asilimia 50-60.

Wakihutubu katika mkahawa mmoja mjini Kisii baada ya kumaliza mkutano wa siku mbili, katibu mkuu wa chama hicho tawi la Masaba, Meshack Ombong'i, na naibu wake James Oteki, walisema kuwa tume ya TSC ndiyo inayohujumu maslahi ya walimu huku wakisihi mahakama kuu kuingilia kati na kuhakikisha kuwa walimu wanapokezwa nyongeza hiyo ya mishahara.

"Kila mmoja wetu anafahamu kuwa masaibu tunayo yapitia kama walimu ni mengi, lakini tume ya TSC ndiyo inayo hujumu pakubwa hatua yetu yakutaka kuongezwa mishahara. Hata hivyo, natumai kuwa mahakama kuu itawahakikishia walimu haki kwa kuhakikisha nyongeza hiyo ya mishahara inatekelezwa," alisema Ombong'i.

Kwa upande wake, naibu katibu wa chama hicho tawi la Masaba James Oteki alisema kuwa anatumai kuwa Mahakama Kuu itaamuru tume ya TSC kuwapokeza walimu nyongeza hiyo ya mishahara akitishia kuwa iwapo mahakama hiyo haitowahakikishia walimu haki, basi itawabidi walimu kugoma kwa mara nyingine.

"Tunajua kuwa kuna watu wanaotaka kuhujumu haki za walimu lakini tunatumai kuwa mahakama kuu itatuhakikishia haki kulingana na yale tunayohitaji kuafikiwa. Iwapo hilo halitaafikiwa, basi tutakuwa tayari kuandaa mgomo kwa mara nyingine," alisema Oteki.