Huenda walimu wa shule za umma katika Kaunti ya Nyamira wakalazimika kutia sahihi kandarasi ya utendakazi wao.
Haya ni kulingana na mkurugenzi wa maswala ya elimu katika Kaunti ya Nyamira John Odongo aliyekuwa akihutubia zaidi ya walimu wakuu 200 wa shule za upili katika shule ya upili ya Menyenya wakati wa hafla ya kuwaeleza walimu hao umuhimu wa utiaji sahihi kandarasi hiyo siku ya Jumatano.
Odongo aidha aliwahimiza walimu wakuu kutia sahihi kandarasi hiyo kabla ya walimu wengine kufuata mkondo, huku akihoji hatua hiyo itaisaidia tume ya uajiri wa walimu nchini kuthathmini utendakazi wa walimu.
"Kuliko siku za hapo awali ambapo walimu wakuu wangetathmini utendakazi wa walimu wao kisiri, sasa mara hii mambo yatakuwa tofauti kabisa kwa kuwa sasa utatia sahihi kandarasi ya utendakazi utakuwa wazi kwa kila mmoja kati ya mutathmini na mthathmiwa," alisema Odongo.
Hata hivyo huenda walimu wakapata changamoto ya kutekeleza agizo hilo kwa maana kwa muda sasa chama cha kutetea maslahi ya walimu nchini kimekuwa kikiwaonya wanachama wake dhidi ya kutia sahihi kandarasi hiyo kwa kile wanachosema kwamba kuna masuala tata yanayostahili kusuluhishwa kabla ya kandarasi hiyo kutiwa sahihi.