Share news tips with us here at Hivisasa

Afisa wa elimu katika Kaunti ya Kisii Charles Nyaribo amesema walimu wa shule za serikali hujihusisha na biashara zao binafsi kando na kufunza, jambo ambalo lilipelekea shule hizo kufanya vibaya katika mitihani ya kitaifa.

Hii ni baada ya shule nyingi za serikali kufanya vibaya katika mitihani ya kitaifa, haswa shule za msingi, kufuatia matokeo ya mitihani yaliyotangazwa ya darasa la nane juma lililopita.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Kisii mnamo siku ya Jumatatu, Nyaribo alisema asilimia 70 ya walimu huwa hawaendi shuleni kila siku, huku wakisalia kufanya biashara zao, jambo ambalo lilipelekea shule nyingi kutofanya vizuri katika mitihani ya kitaifa.

“Shule za serikali haswa katika Kaunti yetu ya Kisii hazikufanya vizuri katika mtihani wa darasa la nane mwaka jana kwa sababu idadi nyingi ya walimu hushughulikia biashara zao binafsi kando na kuenda shuleni kuwasomesha wanafunzi,” alisema Nyaribo.

Wakati huo huo, Nyaribo aliomba kila mwalimu kujaribu kutokosa shuleni kwanzia mwaka huu ili kuhakikisha matokeo ya mwaka huu yanapanda kutoka kiwango yaliko kwa sasa ili Kaunti ya Kisii iwe moja wapo ya kaunti ya kufanya vyema katika mtihani ya kitaifa.

Jukumu ni sekta ya elimu kufuatilia kila mwalimu anafanya kazi yake kunavyostahili kila siku ili kumaliza matokea mabaya katika shule za serikali.