Viongozi wa chama cha kutetea maslahi ya walimu nchini Knut kule Masaba wamejitokeza kuwaomba walimu nchini kujitokeza kuunga mkono hatua ya chama hicho kutaka kubuni chama cha kisiasa.
Wakiongozwa na naibu katibu wa chama cha Knut tawi la Masaba James Oteki viongozi hao walisema wana mipango yakuwasilisha pendekezo lao kwa afisi kuu ya chama cha walimu kule Nairobi ili wabuni chama cha kisiasa kitakachowasaidia walimu kupigania haki zao.
"Kama walimu wa taifa hili yafaa tubuni chama cha kisiasa kitakacho pigania haki za Wakenya wa matabaka yote kwa maana kwa miaka mingi viongozi wa kisiasa wamekuwa wakihujumu haki za wananchi na sharti tujitokeze kuhakikisha hali hiyo imerekebishwa," alisema Oteki.
Kwa upande wake katibu wa chama hicho tawi la Masaba Meshack Ombongi alisema kuwa cha hicho cha kisiasa kitasaidia pakubwa kupunguza visa vya ufisadi nchini ikizingatiwa kwamba serikali iliyoko imekuwa ikipalilia ufisadi nchini.
"Wengi wa walimu nchini ni wanachama wa Knut na kwa kweli tunahitaji watu kama hao ili kusaidia kuthibiti visa vya ufisadi nchini na hata pia kusaidia kupigania haki zetu," aliongezea Ombong'i.
Viongozi hao walikuwa wakihutubia baadhi ya wanachama wa chama cha Knut katika shule ya upili ya Mochenwa siku ya Jumatano.