Share news tips with us here at Hivisasa

Kuna haja ya kuwepo na ushirikiano mwema baina ya walimu, wazazi na wanafunzi ili kuona kwamba viwango vya elimu vinaimarishwa.

Mkurugenzi mkuu wa tume ya kuajiri walimu nchini TSC katika kaunti ya Mombasa Ibrahim Rugut aliyasema hayo wakati wa mkutano na walimu wakuu wa shule za upili na msingi za umma. 

Akiongea na wanahabari afisini mwake mjini Mombasa siku ya Jumatatu, Rugut amesema kuwa iwapo ushirikiano huo utaimarsihwa zaidi basi matokea ya mitihani ya kitaifa katika kaunti ya Mombasa yatakuwa na matokeo bora.

Rugut alisema kuwa juhudi za tume hiyo kutatua mizozo ya mishahara ya walimu inaendelea kukamilika ili kuona kwamba walimu wanawajibikia majukumu yao vyema na kuimarisha viwango vya elimu.

"Tumeona ipo haja ya walimu, wazazi na wanafunzi kushirikiana kwa karibu mno ili kuinua viwango vya elimu kwani hatua hiyo itahakikisha kuwa mambo ya uwajibikaji wa walimu unafanyika sawa," alisema Rugut.

Wakati uo huo amewahimiza walimu wakuu wa shule za upili na msingi za umma kuwajibikia utendakazi wao na kuhakikisha kuwa suala la elimu linaboreshwa katika shule zote za umma.

Rugut aliyazungumza hayo wakati wa kuongoza shughuli ya kutia saini ya kandarasi ya utendekazi ya walimu wakuu wa shule za upili za umma kaunti ya Mombasa.