Wazazi na walimu katika shule spesheli nchini wanataka masomo katika shule hizo kutolewa bila malipo.
Wazazi ambao watoto wao wanasomea katika shule hizo walidai kuwa masomo katika shule hizo ni ghali. Kulingana nao, gharama ya juu ya masomo spesheli ni miongoni mwa mambo ambayo hufanya wazazi wengi kukosa kuwapeleka watoto wenye mahitaji spesheli shuleni.
Msimamo wa wazazi hao uliungwa mkono na muungano wa walimu katika shule spesheli. Muungano huo unataka masomo spesheli kwa wanafunzi lengwa kuanza kutolewa bila malipo.
Mmoja wa viongozi wa muungano huo Cecilia Kebenei alisema iwapo serikali itabuni sera ya kuanza kutoa mafunzo hayo bila malipo kama ilivyo katika shule za misingi za uma wanafunzi wengi watanufaika.
Kebenei ambaye ni mwalimu mkuu wa shule ya watoto wenye changamoto ya kusikia ya Kapsoya mjini Eldoret alisema ingekuwa bora zaidi iwapo mpango wa serikali wa elimu bila malipo FPE ungelenga kwanza shule spesheli.
“Gharama ya kuelimisha watoto wenye mahitaji spesheli iko juu ukilinganisha na watoto ambao hawana mahitaji” alisema Kebenei.
Kiongozi huyo aliongeza kuwa itakuwa bora iwapo serikali itagharamia masomo katika shule spesheli.
Akihutubu shuleni mwake wakati wa kupokea msaada wa vyakula na fedha kwa wanafunzi wake kutoka kwa kilabu ya wamiliki wa magari aina ya Mercedes Benz, Kebenei aliwataka wazazi kuacha kubagua watoto ambao wana ulemavu.
Kebenei alisema ubaguzi dhidi ya watoto walemavu ungali uko juu. Pia alitaka mashirika mbalimbali kushirikiana na wadau wengine katika sekta hiyo kuelimisha wazazi kuhusu umuhimu wa kutunza vyema watoto wa aina hiyo.
Wakati huo huo mwenyekiti wa chama cha walemavu kaunti ya Uasin Gishu Barnabas Chemase alitaka bunge kupitisha sheria kuhusu ulemavu ambayo ilifanyiwa marekebisho.
Chemase alisema iwapo sheria hiyo itapitishwa na kuanza kutekelezwa itawafaa walemavu zaidi walemavu wa matabaka yote.