Wanaume nane kutoka mtaa wa Obunga jijini Kisumu, mnamo siku ya Ijumma walishtakiwa kwenye mahakama ya Winam jijini Kisumu baada ya kunaswa wakiwa walevi huku wakipiga mayowe na kutatiza amani.
Nane hao ambao ni Maurice Rahama, Bethwel Otieno, Ezekiel Ojija, Convice Omondi, George Ouma, Lavins Odhiambo, Daniel Miwaya na Leonard Otieno walinaswa na maafisa wa polisi majira ya saa saba usiku siku ya Alhamisi wakiwa wamelewa chakari mtaani Obunga.
Mahakama iliambiwa kuwa walikuwa wakipiga mayowe, hivyo kuwakosesha amani na utulivu wakaazi wa mtaa huo.
Walikiri mashtaka mbele ya Hakimu Josephine Mitey, na kuomba msamaha mahakamani.
Walipokezwa faini ya shilingi mia tano kila mmoja, au kifungo cha wiki mbili.