Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Mradi wa kunyunyizia maji mashamba wa Galana- Kulalu unaotekelezwa katika Kaunti za Tana river na Kilifi utapelekea kupungua kwa bei ya unga wa mahindi hadi shilingi 84 kwa kipimo cha kilo mbili.

Waziri wa unyunyizaji maji mashamba na raslimali za maji Eugene Wamalwa amesema kuwa mradi huo utakamilika ifikapo mwezi Septemba mwaka huu na utaongeza nafaka katika ghala la serikali, hivyo basi kupunguza gharama ya unga wa mahindi.

Akizungumza mjini Mombasa baada ya kukutana na viongozi wa kaunti za pwani siku ya Jumamosi, Wamalwa alisema kuwa ni lazima mradi huo upewe msukumo zaidi ili ukabiliane na bei ya juu ya unga wa mahindi pamoja na kubuni nafasi za ajira kwa wapwani.

“Serikali inatekeleza jukumu la kuhakikisha kuwa bei ya unga wa mahindi nchini inapungua, na matumaini yetu ni kuhakikisha kuwa tunapata mavuno mengi katika mradi wa Galana – Kulalu ili ghala la serikali kuwa na chakula kingi,” alisema Wamalwa.

Waziri huyo ameyadokeza hayo baada ya ziara yake katika shamba hilo la hekari milioni moja ambapo mradi huo unaotokelezwa na Wahandisi kutoka nchini Israeli umekumbwa na vikwazo vingi na kupelekea mavuno machache.