Share news tips with us here at Hivisasa

Huku wanasiasa wakiweka juhudi za kuwaomba wakazi kuchukua kura kundi la maendeleo ya wanawake kaunti ya Kisii nalo limeanzisha kampeini za kuwahimiza watu kujiandikisha kama wapiga kura katika kaunti ndogo zote 9 mbele ya uchaguzi mkuu wa mwaka uliopita.

Akiongea mjini Kisii siku ya Alhamisi baada ya mkutano, mwenyekiti wa kundi la wamama Bathsheba Sanaya alisema kwamba wameanzisha kampeini hizo baada ya utafiti walioufanya kuonyesha kwamba kina mama na watoto wasichana ambao wamehitimu umri wa kupiga kura hawana hata vitambulisho vitakavyowawezesha kujiandikisha kama wapiga kura.

Bi Sanaya aidha alisema tabia hiyo ya kina mama kupuuza umuhimu wa kujisajili kama wapiga kura ndio sababu kubwa ya idadi ndogo ya viongozi kina mama katika serikali zetu.

Wakati uo huo, kina mama kutoka kaunti ndogo ya Bobasi wameombwa kuanzisha vikundi na kuvisajili ili wapate nafasi nzuri ya kunufaika na fedha za kujiendeleza kupitia kwa miradi pamoja na biashara kutoka kwa serikali ya kaunti pamoja na mashirika mengine.

Bi Norah Moraa Nyamwamu ambaye ni mkurugenzi wa chuo kikuu cha Africa Nazarene kaunti ya Kisii naye alisema kwamba vikundi ni njia moja ya kupigana na umaskini katika maeneo mengi kwa kuwa vinawapatia kina mama njia ya kujitafutia riziki yao ya kila siku.