Wamiliki wa nyumba mtaani Ronda sasa wanatishia kutolipa kodi iwapo serikali ya Kaunti ya Nakuru haitashugulikia miundo msingi mtaani humo.
Wakiongea na mwandishi huyu Jumatano hii mtaani humo, wamiliki hao walisema kutokua kwa miundo misingi kama vile mifereji ya kuondoa maji machafu huchangia pakubwa kufurika mtaani humo punde tu kunapoanza kunyesha.
Walisema mafuriko ya mara kwa mara mtaani humo yamesababishi wapangaji kuhama, hivyo basi kusababisha hasara kubwa kwa miliki wa nyumba.
Wamiliki hao waliokua na ghadhabu walisema kuwa mtaa wa Ronda ndio mtaa ambao hutoa kodi ya pesa nyingi sana mjini Nakuru, lakini haunufaiki kwa vyovyote na kodi hiyo.
Mzee Kamau Maina, ambaye ni mmiliki wa nyumba mtaani Ronda, alisema iwapo serikali ya Kaunti ya Nakuru haitashugulikia miundo msingi mtaani humo, basi hata wao hawatatoa kodi kwani wapangaji wanahama kutokana na mazingira machafu .
"Tutatoa wapi pesa za kulipa serikali ikiwa wapangaji wanahama kutokana na mazingira machafu, sisi tumesema iwapo serikali haitaunda miundo msingi hapa, basi nao pia wasituulize kodi," alisema Maina.
Moreen Njeri, ambaye pia ni mmiliki wa nyumba, alisema tangu mvua ya El-nino kuanza, nyumba zake zimebaki bila wapangaji, kwani wengi walihama wakihofia mpurupuko wa kipindu pindu na mafuriko.
Alisema kati ya nyumba kumi na sita ambazo anamiliki, tatu tu ndizo ziko na wapangaji.
"Ni lazima serikali ielekeze maji kwingineko, tumepata hasara kubwa kwani wapangaji wamehama kutokana na kutokua kwa miundo msingi bora mtaani humu," alisema.
"Tumeamua kama wamiliki wa nyumba hapa Ronda kuwa iwapo serikali inataka tuendelee kulipa kodi, ni lazima nayo iunde miundo msingi ndiposa nyumba zetu ziwe na wapangaji ambao watatupea pesa za kulipa serikali," aliongeza.