Halmashauri ya kuthibiti mazingira nchini, NEMA, imetakiwa kuwachukulia hatua kali wamiliki wa vituo vya kuosha magari mjini Nyamira kwa kuendelea kuchafua mazingira ya mito kwenye eneo hilo.
Akihutubu kwenye hafla iliyoandaliwa na halmashauri hiyo mjini Nyamira, mtaalamu wa mazingira Wellington Ombasa alishangazwa na hatua ya wamiliki wa vituo hivyo vya kuoshea magari wa wamiliki wa majengo ya kibiashara kuachilia uchafu kuingia kwenye mito ya sehemu hiyo, huku akiongeza kusema kuwa ikiwa hali hiyo itaendelea bila hatua mwafaka kuchukuliwa, huenda maji ya mito ya sehemu yasiwe mazuri kwa matumizi ya nyumbani.
"Inashangaza kwamba wamiliki wa vituo vya kuoshea magari na wale wamiliki wa vyumba vya kibinafsi wanaendelea kuachilia uchafu kwenda kwa mito, na inafahamika wazi kuwa mifugo na binadamu hutegemea sana kunywa maji kutoka mito hiyo ambayo watu wangine wanaendelea kuichafua," alisema Ombasa.
Ombasa alisema kuwa uharibifu na uchafuzi wa mito ni swala linalofaa kuangaziwa kwa dharura kwa kuwa uchafuzi huo unaweka maisha ya binadamu kwenye hatari ya kuambukizwa magonjwa mbalimbali, huku akisisitiza kuwa waosha magari hao wanao chafua mazingira wanaweza kuchukiliwa hatua kali kwa mujibu wa sheria.
"Hili swala la uchafuzi wa maji linafaa kuangaziwa kwa dharura kwa kuwa liwaweka maisha ya watu kwenye hatari ya kuambukizwa magonjwa mbalimbali, na waosha magari wanaochafua mazingira wanaweza chukuliwa hatua kali za kisheria kwa uchafuzi huo wa mito," alisisitiza Ombasa.