Huku mvua ikiendelea kunyesha na kusababisha madhara nchini, haswa katika baadhi ya sehemu za Gusii, wamiliki wa manyumba za kukodisha mjini Kisii wamehimizwa kuweka vizuia radi.
Hii ni baada ya watu watatu kupigwa na radi katika kaunti ya Kisii kwa siku chache zilizopita huku wengine wawili wakijeruhiwa katika Kaunti ya Nyamira.
Akizungumza na mwandishi huyu wa habari afisini mwake siku ya Alhamisi, mkurugenzi mkuu wa Idara ya hali ya anga katika kaunti ya Kisii, Henry Sese alisema wamiliki wa nyumba za kukodi wanastahili kuweka vizuia radi ili kuepuka madhara ambayo yanaweza sababishwa na radi.
“Naomba wanaomiliki nyumba kujali maisha ya wale wanaokodisha nyumba zao kwa kuweka vizuia radi, ili kuzuia kuathirika kufuatia mvua inayoendelea kunyesha. Watu wamepoteza maisha yao hapa Kisii baada ya kupigwa na radi kwahivyo ni muhimu kuzuia maafa zaidi,” alisema Sese.
Aliongeza “Ushauri wangu ni kwamba wamiliki wa nyumba hizo wanastahili kuweka vizuizi hivyo ili tukabiline na madhara ya mvua.”
Aidha, aliwataka wakazi kujiepusha na kujikinga mvua chini ya miti na kuwaomba kuwa makini msimu huu wa mvua.