Wamiliki wa pikipiki katika Lokesheni ya Mwamonari, Wadi ya Sensi, wameonywa dhidi ya kuwahusisha vijana wasio na vitambulisho katika biashara hiyo.
Haya yanajiri baada ya idadi kubwa ya wazazi katika lokesheni hiyo kulalamikia wanao kuhusishwa katika biashara hiyo kabla ya kumaliza masomo na hata kupata vitambulisho.
Akizungumza na mwandishi huyu afisini mwake katika eneo la Sombogo siku ya Jumatatu, chifu wa lokesheni hiyo Titus Nyachachi, aliwaonya wamiliki wa pikipiki dhidi ya kuwapa kazi vijana wasio na vitambulisho kwa kusema kuwa watakabiliwa na mkono wa sheria na kuchukuliwa hatua kali.
“Naomba wanye pikipiki kuwakabidhi watu wazima wenye vitambulisho pikipiki ili kufanyia biashara. Yeyote atakayepatikana akimwajiri mwanafunzi atachukuliwa hatua kali ya kisheria,” alisema Nyachachi.
Aliongeza “Sheria hairuhusu mtoto wa shule ama asiye na kitambulisho kuhusishwa na mambo ya uajiri kwa kuwa ni kukiuka sheria.”