Share news tips with us here at Hivisasa

Wafanyibiashara katika vibanda vya Juakali kwenye barabara ya Assis mjini Eldoret wameelezea hofu ya kutokea kwa mkurupuko wa maradhi.

Hofu hiyo inatokana na tabia ya wamiliki wa majumba ya biashara katika eneo hilo kuachilia maji taka kuelekea katika vibanda vyao. Wafanyibiashara hao walidai kuwa maji hayo huwasababishia hasara kubwa mbali na kuwa tishio kwa afya yao na wateja wao.

Walioathiriwa pakubwa ni mafundi wa juakali ,wamiliki wa vibanda vya kuuza vyakula miongoni mwa wengine.

Mwenyekiti wa muungano wa wanabiahara hao Wilfred Omolo alisema juhudi za kushauriana na wamiliki wa majumba hayo kuhusiana na utata huo zimekuwa zikigonga mwamba kutoaka na tabia ya wamiliki husika kuwapuuuza.

“Kila mara tunapowauliza wamiliki wa nyumba husika chanzo cha maji haya wao hutupuuza hata juhudi za kutaka usaidizi kutoka kwa mwakilishi wa wadi hii katika bunge la kaunti hazijafaulu,” alisema Omolo.

Omolo alisema maji hayo hurudisha nyuma biashara yao mbali na kuwa na hatari kwa afya yao.

“Tukiingia asubuhi wao hufungulia maji ambayo ni chafu, tunapofanyiakazi katika mazingira hayo tunatishia afya yetu, hata baadhi yetu wameanza kuwa na ugonjwa wa kukohoa na kuhara kila mara ambapo tunashuku umetokana na maji haya,” aliongeza.

Juhudi za kupata wamiliki wa majengo hayo hazikufaulu kwani wote walidinda kusema lolote kuhusiana na hali hiyo. Kwa sasa wametoa wito kwa idara ya mazingira katika kaunti ya Uasin-Gishu kuingilia kati ili kushawishi wamiliki wa majengo husika kuheshimu sheria za utunzi wa mazingira.

Waziri wa mazingira katika kaunti hiyo Bi Ann Njogu aliahidi kuchunguza madai hayo na kuchukulia wahusika hatua za kisheria.