Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Kufuatia shutuma kali kutoka kwa naibu gavana wa Kaunti ya Kisumu kuwa chama cha Cord hakithamini wanawake, baadhi ya wanaharakati wa mambo ya siasa katika jiji la Mombasa wamepinga madai hayo wakisema kuwa chama hicho cha upinzani kina mtazamo mwema kwa wanawake ikilinganishwa na chama cha Jubilee.

Wakiongozwa na hezekiel Raro wa bunge la mwananchi kwenye mahojiano siku ya Jumatano katika eneo la Mwembe Tayari wanakoendeshea shughuli zao za bunge la mwananchi, wanaharakati hao walidai kuwa Odinga anawapotosha wakenya kwa madai hayo, na kuongeza kuwa haki imezingatiwa vilivyo katika uteuzi wa wanawake na chama hicho cha upinzani.

Raro alitoa mfano wa manaibu wa magavana wanawake akisema kuwa kwa idadi ya manaibu hao tisa, saba ni wa chama cha upinzani cha CORD ikilinganishwa na manaibu wa gavana wawili wa chama cha Jubilee.

“Mimi simuungi mama Odinga mkono, sababu ukiangalia idadi kubwa ya manaibu wanake wa magavana ni wa chama cha Cord, tukianzia na hii Kaunti yetu ya Mombasa tuna mama Hezel Katana, huku Kisumu, Kwale, Taita Taveta, Makueni na Kitui, na Jubilee wana wawili tu huko Embu na Kericho,” Raro alithibitisha.

Hata hivyo, baadhi ya wananchi ambao walizungumza na huyu mwandishi walihisi kuwa vyama vyote bado havijawapa wanawake nafasi mwafaka ya kazi inavyoeleza katiba kuhusiana na thuluthi moja, na kutaka wasimamizi wakuu wa maswala ya kutekelezwa kwa katiba kupitia kwa serikali kuu kujaribu kuwapa wanawake haki stahili.