Mwenyekiti wa chama cha walimu Kenya National Union of Teachers (KNUT) tawi la Gucha kaunti ya Kisii Samuel Nyairo amesema walimu wa chama hicho katika kaunti ya Kisii hawatakubali kutia sahihi mkataba wa kufanya kazi kati yao na tume ya kuajiri walimu nchini TSC hadi tume hiyo iandae kikao kuzungumzia sahihi hiyo inahusu nini na kiiini cha kutia sahihi.
Hii ni baada ya tume ya TSC kusema kuwa walimu watahitajika kutia sahihi mkataba wa kufanya kazi ili kuwa rahisi kwao kuchunguza walimu jinsi wanafanya kazi katika shule mbalimbali jambo ambalo limepingwa na baadhi ya walimu kutoka kaunti ya Kisii.
Akizungumza na waandishi wa habari siku ya Alhamisi mjini Kisii, mwenyekiti wa chama cha KNUT tawi la Gucha Samuel Nyairo alisema liwe liwalo walimu wa kaunti ya Kisii hawatatia sahihi na tume ya TSC .
Nyairo alisema sharti tume ya TSC ijali maslahi ya walimu kwanza kabla ya kuhitaji sahihi zao kwani ni haki yao kukataa kutia sahihi ya maelewano ya kikazi na tume hiyo.