Share news tips with us here at Hivisasa

Wanachama tisa wa kundi ambalo limekuwa likigonga vichwa vya habari eneo la Pwani la MRC kutoka katika kijiji cha Lungalunga wamejisalimisha kwa serikali.

Wanachama hao wanasema kuwa walichukua hatua hiyo kutokana na imani yao kwa serikali kuhusu maswala ya maendeleo.

Tukio hilo lilitokea siku ya Alhamisi wakati wa mkutano huko Lungalunga ulioandaliwa na mshirikishi wa usalama ukanda wa Pwani Nelson Marwa kujadili maswala ya usalama.

Wakiongozwa na Omar Abdala, wanachama hao wanasema kuwa wameamua kuwa raia wema baada ya kundi hilo kuhusishwa na visa vya uhalifu.

“Niliangalia nikaona serikali inaleta maendeleo eneo letu na ndio maana nimeona ni bora nijisalimishe ili niwe raia mwema,” Alisema Omar.

Kwa upande wake Marwa alipokea vyema hatua hiyo na kuahidi kuwasaidia.

Kundi hilo la MRC limekuwa likihusishwa na visa vya uhalifu tangu lilipotangaza kuendeleza harakati za kutenga eneo la Pwani na kuwa taifa huru.

Hata hivyo, serikali imekuwa ikitoa hamasisho kwa kundi hilo kujitokeza na kujisalimisha na hata baadhi yao wameanza kujiandikisha kama wapiga kura ili kushiriki katika uchaguzi mkuu ujao.

Picha: Wanachama wa MRC katika mkutano wa awali. Wanachama wengi wa kundi hilo walijisalimisha siku ya Alhamisi katika hafla moja mjini Mombasa. africajournalismtheworld.com