Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Wanafunzi wawili wa chuo kikuu cha Moi bewa la Annex la taaluma ya uanasheria ni miongoni mwa watu 20 ambao walinaswa katika msako dhidi dawa za kulevya na pombe haramu.

Wanafunzi hao walinaswa katika kituo cha biashara cha Annex karibu na chuo hicho kwenye msako ambao uliendelezwa na bodi ya kukabiliana na pombe haramu na dawa za kulevya katika kaunti ya Uasin-Gishu.

Msako huo uliongozwa na mkurugenzi wa bodi hiyo Armstrong Rono ambaye aliutaja mtaa wa Annex kuwa miongoni mwa mitaa maarufu kwa uhalifu mjini Eldoret kutokana na ongezeko la dawa za kulevya na biashara haramu mtaani humo.

"Visa vya uhalifu katika mtaa huu vimeongezeka kutokana na ongezeko la dawa za kulevya na pombe haramu na zile pombe za bei ya chini ambapo wafanyibiashara husika wanalenga wanafunzi,kama bodi hatutalegeza kamba katika vita dhidi ya dawa hizi na pombe haramu," alisema Rono.

Watu wengine walinaswa katika mtaa wa Sukunanga kwa kupatikana kama wamefungua baa zao kabla ya masaa yaliowekwa kwa mujibu wa sheria.

Rono alionya kwamba bodi hiyo italazimika kufunga baa ambazo hupuuza sheria za kudhibiti pombe hata kama zina leseni za kuuza pombe. Afisa huyo aliamrisha kufungwa kwa baa zote ambazo haziko umbali wa mita 300 kutoka katika shule.

"Sheria imeelezea wazi kwamba baa zapaswa kuwa mita 300 mbali na shule lakini kuna baadhi ya wafanyibiashara ambao hawajali sheria hiyo watu kama hao hatuna mazungumzo nao ila kufunga baa zao bila kusita," aliongeza.