Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Wanafunzi wa vyuo vikuu na taasisi zingine za masomo kutoka eneo bunge la Kitutu Chache kaskazini, Kaunti ya Kisii wamemwomba mbunge wa eneo hilo Jimmy Angwenyi kuongeza kima cha hela wanachopokezwa kutoka akiba ya basari ya karo vyuoni.

Akizungumza na mwandishi huyu siku ya Jumanne mjini Marani, kiongozi wa chama cha wanafunzi kutoka eneo bunge hilo James Mokua alisema kiwango cha pesa wanachokabidhiwa ni kidogo mno kulingana na ulipaji wa karo katika vyuo vikuu na katika taasisi.

Mokua alimwomba mbunge wao kuongeza pesa hizo hadi kati ya shillingi 10,000 na 15,000 kwa kila mwanafunzi wa chuo kikuu kwani kiwango wanachopokezwa ni kidogo, na ambacho ni kati ya shillingi 4,000 na 5,000.

Wakati huo huo, kiongozi huyo aliomba wanasiasa wote kujitolea kutoa usaidizi kwa wanafunzi ambao wanahitaji kusoma lakini hawana uwezo ili kuwafadhili kimasomo kwani elimu ndio msingi wa maisha.

“Tunaomba wanasiasa kujiunga pamoja ili kutoa ufadhili kwa wanafuinzi wale wanahitaji kusoma maana kuna wanafunzi katika eneo bunge hili wanahitaji kuendeleza masomo lakini hawana wa kuwafadhili na kuendelea na elimu,” alisema Mokua.

“Pia naomba mbunge wetu Angwenyi aongeze kiwango cha pesa za basari ili sisi vijana tuendelee na masomo tuje kujisaidia nyakati sijazo,” aliongeza Mokua

Aidha, kiongozi huyo aliomba uwazi kuonekana wakati pesa hizo za basari zinagawa kwa wanafunzi wa shule na vyuo vikuu.