Huku viongozi wa wanafunzi wa chuo kikuu cha anuwahi cha Mombasa pamoja na wanafunzi ambao walishiriki katika ghasia mwezi jana wakikamilisha kutoa ushahidsi wao mbele ya kamati ya kinidhamu ya chuo hicho siku ya Jumanne, wanafunzi wametakiwa kuwa na subira wanapongojea uamuzi wa kamati hiyo.
Kwenye mahojiano na naibu kiongozi mkuu wa wanafunzi wa chuo hicho Dennis Oseko siku ya Jumanne mjini Mombasa, kiongozi huyo alisema kuwa wanafunzi pamoja na viongozi wao wanahitajika kuwa na umoja ili kuendeleza taaluma ya kila mmoja, ikizingatiwa kuwa hicho ndicho chanzo na kiunganishi kikuu kilichowaleta pamoja kwenye chuo.
Shughuli hiyo ambayo ilianza siku ya Jumatatu ilikimalika siku ya Jumanne, huku viongozi wa wanafunzi na wanafunzi wakienda mbele ya kamati ya chuo hicho ya kudhibiti nidhamu.
Hatua hiyo inajiri baada ya viongozi wote wa wanafunzi kupewa barua wiki jana za kupigwa marufuku kuingia chuoni kwa kile kinachodaiwa kuwa walishiriki kuwachochea wanafunzi kutolipa shilingi 2,650, ambazo kila mwanafuzi alihitajika kulipa kama faini kwa kushiriki katika maandamano ambayo yalisababisha kuchomwa kwa malori mawili ya Kaunti ya Mombasa.
Ikumbukwe kwamba awali, wanafunzi hao waliandaa kikao na kamati teule ya bunge la Kaunti ya Mombasa ambalo limejukumika kutathmini kilichojiri kwenye maandamano hayo, na hatua zitakazofuata hasa kuhusiana na kuteketezwa kwa malori ya kuzoa taka ya Kaunti hiyo.