Afisa wa maswala ya mitihani amewahakikishia watahiniwa wa darasa la nane wa wilaya ya Nyamira Kaskazini watakaokuwa wakiufanya mtihani wao mwaka huu kuwa mikakati imewekwa ili kuhakikisha kuwa wanafanya mitihani yao kwenye mazingira tulivu.
Akiongea kwenye shule ya msingi ya Makairo wakati wa hafla ya maombi siku ya Jumatatu kwa wanafunzi hao, afisa wa tume ya kitaifa ya mitihani nchini tawi la Nyamira kusini Julius Tundura alisema kuwa mikakati kabambe imewekwa kuhakikisha kwamba wizi wa mitihani haishuhudiwi, huku akiongeza kusema kuwa yeyote atakayepatikana akijihusisha na visa vyovyote vya wizi atakabiliwa kisheria.
"Mikakati kabambe imewekwa kuhakikisha kwamba mitihani ya mwisho ya darasa la nane haishuhudii visa vyovyote vya udanganyifu, na yeyote atakayepatikana akijihuzisha kujaribu kuiba mitihani hiyo atatiwa mbaroni na kushtakiwa mahakamani," alisema Tundura.
Tundura aidha alisema kuwa tayari maafisa watakaolinda mitihani hiyo wameteuliwa kutoka Knec, Chuo cha mitaala ya silabasi nchini, wizara ya elimu, tume ya uajiri wa walimu na muungano wa walimu wa shule za upili nchini, huku akiwaomba walimu kutojihuzisha na na visa vya udanganyifu kwa kuwa watatiwa mbaroni.
Haya yanajiri baada ya visa vya kuiba mtihani wa kitaifa wa kidato cha nne kudhihirika hadharani, hali iliyosababisha baadhi ya maafisa wa polisi, walimu na wanafunzi kutiwa mbaroni kwa tuhuma zakujihuzisha na wizi huo.