Huku dunia ikiomboleza watu wasiopungua 127 waliouawa katika shambulizi la kigaidi Paris, Ufaransa wanafunzi zaidi ya 4,000 wamepokea mafunzo ya kukabiliana na ugaidi.
Zaidi ya wanafunzi 4,000 wa Chuo Kikuu cha Eldoret hivi leo wamepokea mafunzo maalum kuhusiana na mbinu za kukabiliana na mashambulizi ya kigaidi.
Mafunzo hayo yaliendeshwa na maafisa wa polisi kutoka kitengo cha kukabiliana na ugaidi ATPU kwa kushirikiana na wataalamu wa mabomu.
Wakati wa mafunzo hayo wanafunzi walipata fursa ya kuonyeshwa aina mbalimbali ya mabomu na jinsi ya kuzitambua na kuchukua hatua mwafaka za usalama wakati kunakotokea shambulizi.
Maafisa hao wakiongozwa na James Mirage kutoka ATPU kanda ya Magharibi mwa Kenya walionyesha wanafunzi aina mbalimbali ya mabomu ambayo yalikuwa ni pamoja na guruneti miongoni mwa silaha nyingine hatari ambazo hutumiwa na magaidi.
Mirage aliwataka wanafunzi kuwa macho zaidi na mizigo ambayo huachwa na watu wasiojulikana hasa katika maeneo ya uma na katika taasisi za elimu.
"Unapopata mzigo ambao umeachwa mahali usiwe na haraka ya kuanza kukagua, ni vyema ufahamishe maafisa wa polisi kuhusu mzigo unaoushuku,” alisema Mirage.
Mirage alisema ni maafisa wa polisi pekee ndio wanaruhusiwa kukagua mzigo kama huo kwa tahadhari.
Akizungumza na waandishi wa habari baada ya mafunzo hayo katika Chuo Kikuu cha Eldoret kaimu msajili wa wanafunzi Profesa Donald Otieno alisema mafunzo hayo ni sehemu ya Chuo hicho kutoa mazingira bora ya usalama kwa wanafunzi.
Profesa Otieno alisema tangu wanafunzi zaidi ya 100 wafariki katika chuo kikuu cha Garissa kutokana na mashambulizi chuo hicho kimekuwa kikichukua kila hatua ili kuhakikishia wanafunzi usalama chuoni humo.
"Kama Chuo Kikuu tunachukua kila tahadhari kuhakikishia wanafunzi usalama pamoja na jamii nzima ya chuo hiki,”alisema Profesa Otieno.
Profesa Otieno alitoa wito kwa wakuza mitalaa ya masomo nchini kubuni mitalaa ambayo itawawezesha wananfunzi kuanza kujifunza kuhusu usalama na mbinu za kukabiliana na ugaidi wakiwa wangali chipukizi.
Wakati huo huo viongozi wa wanafunzi kutoka chuoni humo wakiongozwa na kiongozi wao Bw Mandere Obondi walitoa wito kwa utawala wa chuo hicho uwe ukiendeleza mafunzo kama hayo mara kwa mara.
Obondi alisema mafunzo kama hayo yatawahakikishia wanafunzi usalama katika taasisi za elimu kote nchini.
“Wanafunzi wengi wameanza kuwa na uoga kujiunga na vyuo vikuu baada ya lile shambulizi la chuo kikuu cha Garissa mafunzo kama haya yatarejesha imani ya wanafunzi kuhusiana na usalama wao chuoni,” alisema.