Mwenyekiti wa chama cha waandishi wa habari walio Mashinani KCA William Oloo Janak, ametoa wito kwa vyombo vya habari na wanahabari kwa ujumla kuunga mkono ugatuzi.
Akizungumza siku ya Jumatatu kwenye mkutano uliowaleta pamoja wanahabari na wanachama wa mashiriki mbali mbali ya kijamii, ulioandaliwa katika afisi za Kisumu Media and Information Hub mtaani Tom Mboya, jijini Kisumu, Janak alisema kuwa baadhi ya viongozi nchini wanaendelea kupiga vita ugatuzi.
Alisistiza kuwa vita hivyo havitafika mbali iwapo wanahabari wataunga mkono mfumo huo wa uongozi, kwa kuandaa taarifa zinazohusiana na ugatuzi kwa wingi.
“Wanahabari mna jukumu kubwa la kuhakikisha kuwa viongozi kwenye serikali za kaunti wanatekeleza majukumu yao ipasavyo, kupitia kuuliza maswali yanayoambatana na masuala ya uongozi, na matumizi ya pesa za umma katika kiwango cha kaunti,” alisema Janak.
Wadau wa mashirika ya kijamii waliohudhuria mkutano huo, walikiri kuwa pana haja ya kushirikiana zaidi na vyombo vya habari na wanahabari, ili kuwahamasisha wananchi kuhusu ugatuzi na manufaa yake.