Naibu afisa mkuu mtendaji katika baraza la wanahabari nchini Victor Bwire, ameonya wanahabari dhidi ya kutowajibikia majukumu yao ya kuchapisha habari za kuelimisha umma kuhusu maswala ya kimsingi.
Akizungumza katika warsha moja mjini Naivasha iliyowaleta pamoja wanahabari kutoka maeneo mbalimbali nchini siku ya Jumanne, kuhusu mabadiliko ya hali ya anga, Bwire alisisitiza kuwa ni sharti wanahabari wajibidiishe kuwapasha wananchi habari muhimu ya jinsi ya kuchukua tahadhari kabla ya majanga kutokea.
Aidha, alihimiza mamlaka husika kitaifa na katika kaunti kushirikisha wanahabari katika nyanja mbalimbali.
Pamoja na hayo, aliwashauri wanahabari kuzingatia mwongozo na kanuni za wanahabari pasi na kushawishika kwa vyovyote vile.