Wanaharakati wa kutetea maslahi ya ardhi za wananchi nchini, sasa wametenga kuanzisha chama cha kisiasa kitakachoshughulikia masuala ya uskwota ili kusitishwa mizozo ya ardhi nchini.
Mwenyekiti wa Shirika la kitaifa la Ardhi maarufu Residents Land Protection Organisation of Kenya, Dewelly Nyambu alisema kuwa mikakati ya kukamilisha utaratibu wa usajili wa chama hicho unaendelea kukamilika.
Alisema kuwa chama hicho iwapo kitawasilisha wajumbe katika bunge la kitafa baada ya uchaguzi mkuu ujao basi kitaishinikiza serikali kutangaza tatizo la ardhi kuwa janga la kitaifa na kushughulikiwa jinsi ipasavyo ili kusitisha mizozo ya ardhi nchini na kudumisha amani.
Nyambu amesema kuwa kupitia chama hicho maswala ya uskwota nchini na hususan eneo la Pwani utapata suluhu la kudumu ili kuona kwamba kila Mkenya anamiliki ardhi yake sambamba na kuwa na hati miliki za ardhi.
"Tumekubaliana kwa kauli moja kuzindua chama cha kisiasa kitakachoshughulikia masuala ya uskwota na kulishinikiza bunge la kitaifa iwapo wafuasi wetu watachaguliwa ili kusitisha mzozo ya ardhi nchini na hususan eneo la Pwani na Wakenya wapate hati miliki zao za ardhi," alieza Nyambu katika mkutano na wanahabari mjini Mombasa siku ya Alhamisi.
Kauli ya mwanaharakati hio imejiri huku Rais Uhuru Kenyatta akiendeleza ziara yake eneo la Pwani ya kutoa hati miliki za ardhi kwa Wapwani katika juhudi za kutoa suluhu la kusitisha mizozo ya ardhi eneo la Pwani.