Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Baada ya serikali kupendekeza wakazi wanaoishi katika shamba la Waitiki kulipa shilingi 182,000 kama gharama ya kusimamia shughuli za usorovea katika shamba hilo, sasa mgogoro wazuka baada ya maskwota katika shamba hilo lenye ukubwa wa hekari 930 kudidinda kulipa ada hiyo.

Mwenyekiti wa Shirika la ardhi la Land Residents Protection Organization of Kenya, Dewelly Nyambu amesema kuwa pesa hizo zilizotengewa wakazi hao kulipa ni nyingi mno kutokana na changamoto wanazopitia maskwota hao.

Akizungumza mjini Mombasa siku ya Ijumaa, Nyambu amesema kuwa viongozi wanaoshughulikia swala hilo wanafaa kukubaliana vyema na kuwasaidia maskwota hao licha ya kuwa wanahitaji hati miliki hizo.

Wakati uo huo amemtaka Rais Uhuru Kenyatta kusitisha hatua ya utoaji hati miliki elfu tano kwa wakazi hao wa Shamba la Waitiki hadi mgogoro uliopo kuhusu swala la wakazi hao kulipa ada ya shamba hilo kwa kila familia hizo elfu 11 kutatuliwa.

"Tunamwomba Rais Uhuru Kenyatta kusitisha utoaji wa hati miliki za ardhi katika shamba la Waitiki hadi mgogoro uliopo wa kulipa ada ya shilingi elfu 182 kusuluhishwa," alisema Nyambu. 

Kauli ya mwanaharakiti huyo wa kutetea ardhi za wananchi imejiri siku mbili tu baada mgogoro kuzuka katika shamba hilo wakazi wakidinda kulipa ada kama malipo ya kugharimu shughuli za usorovea.